WATU watatu (wanawake 2, mwanaume 1) wamefariki
dunia na wengine 34 wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na
hospitali ya Mburahati jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kipindupindu.
Hospitali ya Sinza Palestina imeripotiwa kuwa na wagonjwa walio na dalili za ugonjwa huo zaidi ya 50.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bw. Paul Makonda amezitaja Kata zilizoathirika na ugonjwa huo kuwa ni Kijitonyama, Kimara, Manzese, Tandale, Saranga, Makumbusho na Mwananyamala.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amesema kuna ripoti ya wagonjwa waliolazwa 71 hadi sasa, na kwamba Wilaya ya Ilala na Temeke bado hazijakumbwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na wanahabari , Jijini Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Minispaa hiyo, Dk. Aziz Msuya, amesema kuwa mgonjwa wa kwanza aligunduliwa katika maeneo ya Kijitonyama kwa Ally Maua na kufia nyumbani kwake katika eneo hilo na kuambukiza ndugu zake wawili ambao walikufa wakati wanapelekwa Hospitali.
Dk. Msuya amesema kumetayarishwa kambi za muda katika Hospitali za Kijitonyama, Mwananyamala na Sinza Palestina pamoja na kambi kuu iliyopo katika Hositali ya Mburahati. Amewataka wananchi wa Jiji hilo kuchukua tahadhari kwa kuweka mazingira safi kunywa maji yaliyochemshwa na kujiepusha kula vyakula vilivyopikwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
“Ukipata huu ugonjwa tutakupa dawa lakini kwa sasa tumetoa dawa katika maeneo yale ambayo tumeona yameathirika zaidi ambayo ni Manzese na Kijitonyama. Tumeshazipa dawa kaya zile ambazo tunazitilia mashaka kwamba zinawezikawa zimepata maambukizi, na wale waliopo katika maeneo mengine ambayo sio maeneo hayo niliyokutajia hapo awali, wanapoona hizo dalili za kutapika na kuhara basi wafanye haraka kukimbia Hospitali.
No comments:
Post a Comment