Friday, May 30, 2014

TANZANIA inapata hasara ya sh. bilioni 301 kila mwaka kutokana na wananchi kutotumia vyoo



IMEELEZWA kuwa Tanzania inapata hasara ya shilingi bilioni 301 kila mwaka, sawa na bajeti za wizara mbili, kutokana na wananchi wake zaidi ya milioni tano kutotumia vyoo, na hivyo kusababisha magonjwa ya milipuko yanayoweza kuzuilika.

Akiwasilisha taarifa ya utafiti uliofanywa na Benki ya dunia, Meneja Mipango na Uendeshaji wa Mradi wa Usafi wa Mazingira Tanzania, mhandisi Koronel Kema, amesema kutokuwepo kwa usafi wa mazingira kunailetea nchi hasara kwa kuyatibu magonjwa yanayotokana na uchafu badala ya kuyazuia.

Mhandisi Kema amebainisha leo na kusisitiza kuwa kutokuwepo kwa usafi wa mazingira kunachangia vifo, ambapo inakadiriwa watanzania zaidi elfu 20 kati yao wakiwemo watoto elfu kumi na nane hupoteza maisha.

Awali akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi. Betty Mkwasa amesema pamoja na wilaya anayoiongoza kuwepo katika mradi wa ujenzi wa vyoo bora bado serikali wilayani humo imetenga siku moja ya usafi katika wiki, kabla ya watu kwenda kufanya shughuli nyingine za maendeleo, baada ya kutambua umuhimu wa kutunza mazingira.


Mradi wa usafi wa mazingira Tanzania (UMATA) unaosimamiwa na Plan International, unatekelezwa katika wilaya tatu za mkoa wa Dodoma, ambayo ni Bahi, Kongwa na Chamwino, huku lengo la mradi huo likiwa kuwahamasisha wananchi kutumia vyoo bora na kujenga tabia ya kunawa mikono, kabla ya kula na wanapotoka chooni.
-------------------------------------------
     

MAADHIMISHO ya 17 ya wiki ya Maziwa  kitaifa yamezinduliwa leo mkoani Mara ambapo imeelezwa  kuwa kiwango cha unywaji Maziwa bado ni kidogo ikilinganishwa na kile kilichopendekezwa na Shirika la Chakula na Afya Duniani.

Mwakilishi wa Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mara Bw Jackson Msome ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Musoma ameyasema hayo katika uzinduzi wa maadhimisho ya 17 ya wiki ya Maziwa katika uwanja wa Shule Msingi Mukendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.  

Amesema lengo la Maadhimisho hayo ni kulenga shughuli za wadau wa Maziwa ingawa kuna changamoto kubwa kwa viwanda vya usindikaji Maziwa nchini huku akisema kuwa kutokana na uzalishaji kwa sasa wastani wa unywaji Maziwa kwa mtu  ni lita 45 kwa mwaka  huku viwango vilivyopendekezwa na Shirika la WHO na FAO ni kunywa Maziwa lita 200 kwa mwaka. 

Katika Maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni june mosi mwaka huu shirika la taifa la hifadhi ya Jamii NSSF  limeendesha kambi ya upimaji wa afya bure kwa wakazi wa Mkoa wa Mara ambapo litaendesha zoezi hilo kwa siku tatu na baadae kuelekea katika mikoa ya shinyanga, Geita na  Kagera




No comments:

Post a Comment