Friday, July 31, 2015
UN yatoa agizo la kupambana na biashara haramu ya wanyama pori
BARAZA Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kupambana na biashara haramu ya wanyama na mimea pori, na kuzitaka nchi wanachama wa Umoja huo kupambana na vitendo hivyo.
Azimio hilo limesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linafuatilia athari mbaya kwa uchumi, jamii na mazingira zinazoletwa na ongezeko la biashara haramu za wanyama na mimea pori.
Azimio hilo linazitaka nchi mbalimbali zichukue hatua thabiti kuzuia na kuepusha biashara haramu ya wanyama na mimea pori na kuwashawishi wateja wasinunue bidhaa husika.
Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kupasisha azimio maalumu la kukabiliana na ujangili. Imedokezwa katika miaka ya hivi karibuni ndovu 30,000 wamekuwa wakiuawa kila mwaka barani Afrika kutokana na thamani kubwa ya pembe ya mnyama huyo.
Imearifiwa kuwa China inashikilia asilimia 70 ya soko la pembe za ndovu jambo ambalo limepelekea wanyama hao kuangamizwa kwa kasi hasa nchini Tanzania na Kenya.
Azimio hilo limepitishwa siku chache tu baada ya raia wa Marekani kumuua simba mashuhuri sana kwa jina la Cecil nchini Zimbabwe na kutoroka. Kitendo cha Mmarekani huyo aliyetambuliwa kama Daktari Walter Palmer kimeibua hasira ya walimwengu na wasi wasi kuhusu raia kuendelea kuangamiza wanyama pori barani Afrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment