SERIKALI ya Burundi
imesema haitashiriki duru ya pili ya mazungumzo ya amani na upinzani
yanayotazamiwa kuendelea kesho mjini Arusha nchini Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje ya Burundi, Joseph Bangurambona, amesema upande wao hautashiriki
kikao cha kesho na cha Januari 16 cha kujaribu kuutafutia ufumbuzi mzozo wa
kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Bangurambona amesema
pande husika hazijakubaliana kuhusu tarehe kamili ya kuendelea na mazungumzo
hayo. Kamisheni ya Umoja wa Afrika imetishia kuziwekea vikwazo pande hasimu za
nchi hiyo ya Afrika Mashariki, iwapo wawakilishi wao hawatashiriki mazungumzo
ya amani mwezi ujao.
Duru ya kwanza ya
mazunguzo hayo ilifanyika mjini Entebbe nchini Uganda chini ya usimamizi wa
Rais Yoweri Museveni. Umoja wa Mataifa umezitaka pande hasimu nchini Burundi
kufikia makubaliano kuhusiana na mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo ambao
umepelekea kutokea mauaji ya kiholela.
Burundi ilitumbukia
katika machafuko na ghasia za ndani baada ya Pierre Nkurunziza kutangaza nia
yake ya kuwania tena kiti cha urais kwa kipindi cha tatu mfululizo hapo Aprili
mwaka huu. Wapinzani wanasema kuwa, uamuzi wa kiongozi huyo ulikiuka katiba ya
nchi na makubaliano ya amani ya Arusha yaliyohitimisha rasmi vita vya ndani vya
Burundi.

No comments:
Post a Comment