Wednesday, July 2, 2014

MKUU wa wilaya awataka wananchi kujiandaa na zoezi la makazi


Mkuu wa wilaya ya Kilosa
WAKAZI wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wametakiwa kujiandaa na zoezi la usajili na utambuzi kwenye daftari la wakazi katika maeneo yao wanayoishi ili kupata kitambulisho cha Taifa ambacho ni muhimu kwa kila Mtanzania aliyefikisha umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.


Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Elias Tarimo ofisini kwake wakati akizungumza kwenye kikao maalum kilichowahusisha Wakuu wote wa Idara na Viongozi mbalimbali Julai mosi mwaka huu.

Tarimo amesema kuwa zoezi la kujisajili na utambuzi kwa wananchi Mkoani Morogoro litazinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera Agosti 4 mwaka huu lengo likiwa kila mwananchi ambaye ni Mtanzania halali aweze kupata kitambulisho cha Taifa.

Hatahivyo amesema kuwa ni jukumu la Maafisa watendaji wote kuhakikisha wananchi wamejiandikisha katika maeneo yao kwenye daftari la mkazi ili kurahisisha zoezi hilo litakapoanza pia amewataka kuacha kudai malipo yoyote kwani kazi hiyo ni wajibu wao.
Zoezi la usajili na utambuzi kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa linaendeshwa na serikali kupitia mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambapo Kitaifa limeanzia Mkoani Dar es salaam na kwa Mkoa wa Morogoro litazinduliwa rasmi mapema mwezi ujao mwaka huu.





No comments:

Post a Comment