Sunday, May 31, 2015

NDEGE aina ya kwereakwerea wavamia mashamba ya mpunga wilaya ya Mvomero



NDEGE wanaosadikiwa kuwa Kwerea kwerea wamevamia mashamba ya mpunga na kula mipunga iliyokuwa imeanza kukomaa katika vijiji vilivyo katika bonde la Mgongola katika kata ya Turiani,Dihombo,Mvomero,Hembeti na kuhatarisha kuibuka baa la njaa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wakiomba msaada wa kuwateketeza ndega hao,Ashura Ramadhani wa Misufini na Jafari Omary wa Dihombo wakiungwa mkono na mwenyekiti wa kijiji cha Misufini Albert Chiloso walisema ndege hao wanaongezeka kwa kasi na kula Mpunga unaoelekea kukomaa.   
“nadhani wanahabari mtatusaidia maana ndege hawa walianza kujitokeza mapema mwezi wa tatu,lakini sasa hivi ni wengi kupita maelezo…kumbuka sasahivi wanashambulia hasa Mpunga unaoelekea kukomaa,kama hatutakuwa tumepata dawa ya kuwaangamiza mapema mwaka huu hatutakuwa na zao hilo huku kwetu”alifafanu  Ashura.
Walisema mbali na kutumia njia za asili ikiwemo kuunganisha makopo na madebe kwenye kamba kisha kuyagonganisha kila baada ya masaa kadhaa na wengine kulazimika kushinda mashambani kuwafukuza juhudi hizo hazionyeshi mafanikio kutokana na ongezeko kubwa la ndega hao.
“tulisha toa taarifa kwenye serikali ya kijiji na taarifa zipo kwenye uongozi wa kata tangu mwezi wa nne lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa wala hatujapata mrejesho wowote labda tusaidieni wenzetu waandishi pengine wakasikia huko juu kinachoendelea’alisema Omary.
Walisema mbali na mazao hayo ya nafaka hususani Mpunga na Mahindi kutumika kwa chakula pia ni mazao yao makuu ya biashara na yamekuwa yakiwasaidia kukabiliana na umasikini pia changamoto za ugumu wa maisha ikiwemo kuboresha makazi na kusomesha.  
Mwenyekiti wa kijiji cha Misufini Albert Chiloso,sambamba na kukili kuwepo kwa ndege hao alisema taarifa zimewasilishwa ofisi ya kata na hawajapata mrejesho wowote licha ya makundi hayo ya ndege kuongezeka kwa kasi.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa hatua zilizochukuliwa kuwakabili ndege hao,Diwani wa kata ya Hembeti Juma Malaja mbali na kukili kuwepo kwa ndege hao alisema taarifa zimefika wilayani na serikali imeshaanza kuchukua hatua ikiwemo kununu madawa na mafuta ya ndege itakayotumika kunyunyiza dawa hiyo.
Katika ufafanuzi wake Malaja alisema ndege iliyopo maalumu kwa kazi hiyo inadaiwa kuwa mkoani Singida kukabili tatizo kama hilo ambapo baada ya hapo huenda ikaelekea mkoani Dodoma na baadae wilayani humo.


No comments:

Post a Comment