KAMPENI mbalimbali za usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo bora shuleni zinazoendelea mkoani singida, zimekuwa zikisisitizwa mara kwa mara na viongozi mbalimbali ikiwa ni moja ya njia ya kunusuru na kusaidia jamii ya Watanzania katika kuepukana na madhara mbalimbali yatokanayo na uchafuzi wa mazingira.
kwa nyakati tofauti, viongozi wa mkoa wa Singida akiwemo Mkuu wa mkoa huo, Dk. Parseko Kone wamekuwa wakisisitiza hilo hususani katika kampeni maarufu za siku ya choo na kunawa mikono na usafi wa mazingira kwa kuwataka wananchi kuzingatia suala la usafi.
Gazeti hili lilifanya utafiti mdogo katika shule mbalimbali mkoani singida zilizopo wilayani Iramba na kubaini kuwa kutokuwa na vyoo bora shuleni imekuwa moja ya sababu za utoro wa mara kwa mara na kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kimasomo kwa wanafunzi hasa wakike ambao wamefikia umri ama wa kubalehe na kuingia katika kipindi cha hedhi.
Akifafanua hali hiyo Dk. Kone alisema “Kukosekana kwa vyoo vyenye miundombinu ya kujisitiri imebainika kuwa kila msichana mwenye umri wa kubalehe hupoteza siku sitini 60 kila mwaka katika masomo yake ambapo hali hii husababishwa na kukosekana kwa miundombinu rafiki katika mazingira ya shule na hali hii inapelekea kurudisha nyuma maendeleo yao kimasomo”.
Kutokana na hali ilivyo katika mkoa wa Singida, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Bi Aziza Mumba aliwaeleza waratibu elimu kata na wakuu wa shule katika warsha ya kutathmini na kujadili miongozo mbalimbali ya kukagua halihalisi ya usafi kuwa hali ni mbaya.
“Kukosekana kwa mifumo ya maji safi katika shule mbalimbali hali ilivyo kwa sasa nchini ni asilimia 38 tu ndizo zenye vyoo vya kutosha, vifaa vya kunawia mikono ambapo pia katika asilimia 20 ya shule ndizo zenye mifumo ya kusambazia maji safi mashuleni,” alisema.
Akifafanua takwimu za kitaifa juu ya hali ya usafi na mifumo ya maji safi katika shule za misingi na sekondari nchini, hali inaonesha ni chini ya asilimia 10 ya shule zote nchini ndizo zenye vifaa vya kunawia mikono vyenye maji wakati wote.
Vilevile alisema imebainika kuwa shule zisizo na mifumo ya maji safi, vifaa vya afya na usafi wa mazingira ndizo zinaongoza kwa milipuko ya magonjwa ambayo huleta madhara zaidi katika mahudhurio na utendaji mbaya kwa wanafunzi pamoja na kuacha kusoma kabisa.
“Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wanaoathirika zaidi ni watoto wa kike wenye umri wa kubalehe na walemavu ambapo kwa wanafunzi wa kike mara zinapofika siku zake za hedhi, hali hiyo humbidi kutokwenda shule na kubaki nyumbani kutokana na miundombinu ya shule kutokuwa rafiki kwao,” alisema.
Mratibu wa Maji na Usafi wa Mazingira (SWASH), Mkoa wa Singida, Suleimani Benjamin Nkondo alizungumzia hatua mbalimbali za Serikali katika kuboresha miundombinu ya vyoo shuleni.
”Mpango wa kitaifa wa Serikali katika kujenga vyoo bora shuleni hapa nchini ni kujenga vyoo hivyo katika shule mbili kwa kila halmashauri zilizopo,” alisema.
Licha ya kuwepo kwa mpango huo wa serikali wa kujenga vyoo shuleni, imebainika kuwa mpango huu utachukuwa muda mrefu katika kufikia viwango vinavyokubalika .
Sababu kubwa ya kushindwa kufikia lengo hilo ni kutokana na uwepo wa shule nyingi katika mikoa yote nchini, ambapo kwa mkoa wa singida takwimu zinaonesha kuwa kuna jumla ya shule 522. Ili kumaliza shule zote itachukua muda mrefu na miaka mingi kumaliza shule zote.
Takwimu za Mkoa wa Singida zinaonesha kuwa kwa sasa matumizi ya choo kwa wanafunzi ni wastani wa tundu moja kwa wanafunzi 60 na baadhi ya shule kubainika kuwa hazina vyoo kabisa.
Hali hii inaonekana kutokuwa na uwiano mzuri katika matumizi ya vyoo katika shule zetu ambapo kwa kiwango cha kitaifa na kimataifa matumizi ya vyoo shuleni ni tundu moja kutumiw
No comments:
Post a Comment