Sunday, June 15, 2014

MANOWARI za jeshi la Iran zaanza safari ya kuelekea nchini Afrika kusini


Manowari ya jeshi la wanamaji wla Jamhuri ya Kiilsamu ya Iran ikielekea Afrika kusini

 MANOWARI za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaelekea Afrika Kusini ikiwa ni utekelezwaji wa sera za Iran za kuimarisha uwepo wa wanamaji wake katika maji ya kimataifa.


Msafara huo wa 30 wa Manowari za Iran tayari umeshamaliza kazi zake katika Ghuba ya Aden, Lango Bahari la Bab el-Mandeb  na katika Bahari ya Sham na ulikuwa katika bandari ya Dar es Salaam Tanzania kwa siku kadhaa kabla ya kuondoka jana Jumamosi na kuelekea Cape Town Afrika Kusini.

Wakati huo huo Balozi wa Iran nchini Tanzania Bw. Mehdi Agha Ja'afari amesema kumefikiwa mapatano ya kuwawezesha askari wa Jeshi la Wanamaji la Tanzania kupata mafunzo nchini Iran.

Akizungumza Dar es Salaam wakati wa kuaga manowari za Iran, ameongeza kuwa wakuu wa Jeshi la Tanzania wametaka kuimarisha ushirikiano zaidi na Iran.

Katika miaka ya hivi karibuni manowari za Iran zimeimarisha doria katika maji ya kimataifa kulinda njia za baharini zinazotumiwa na meli za kibiashara na zile zinazosheheni mafuta ya petroli.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) limelipongeza Jeshi la Wanamaji la Iran kwa mafanikio yake katika kupunguza uharamia baharini.

No comments:

Post a Comment