Monday, February 15, 2016

WATU 51 wafariki kwa ugonjwa wa homa ya manjano nchini Angola

MKUU  wa idara ya Taifa ya afya nchini Angola amesema kuwa, watu 51 wamefariki dunia katika kipindi cha chini ya miezi mwili katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kutokana na homa ya manjano.


Kwa mujibu wa afisa huyo mwandamizi wa afya nchini Angola, watu 240 wamekumbwa na homa ya manjano nchini humo na tayari 51 kati yao wameshapoteza maisha.

Amesema, zaidi ya watu 450 wameshapigwa chanjo ya kuzuia ugonjwa huo katika mji mkuu Luanda, ambacho ndicho kituo kikuu cha kuenea homa hiyo hatari nchini Angola.
Ugonjwa wa homa ya manjano umeenea nchini Angola katika hali ambayo nchi hiyo imekumbwa na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na kuporomoka bei ya mafuta kiasi kwamba hata bajeti ya fedha za kukusanya takataka imefutwa na matokeo yake ni kurundikana taka katika maeneo ya watu maskini au kwenye vituo vya mabasi na kuandaa mazingira ya kuzaliana mbu wanaosambaza virusi vya ugonjwa huo.

Si hayo tu, lakini pia wafanyakazi wengi wa masuala ya afya na usafi nchini Angola wanalalamikia kutolipwa mishahara yao.(Idahaa ya Kiswahili ya redio Tehran, Irib)

No comments:

Post a Comment