Saturday, May 7, 2016

YANGA kuvaana na Sagrada Esperanca ya Angola Uwanja wa Taifa leo


Wachezaji wa Yanga wakishangilia

YANGA leo inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuivaa Sagrada Esperanca ya Angola, ikiwakosa wachezaji wake nyota raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

Kamusoko na Ngoma ni msimu wao wa kwanza Yanga wakitokea FC Platinums ya Zimbabwe, ambapo Ngoma hadi sasa amecheza mechi 45 na kufunga mabao 24 na Kamusoko amecheza mechi 46 na kufunga mabao tisa katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ngoma mwenye mabao matatu aliyofunga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika alioneshwa kadi ya pili ya njano katika pambano la marudiano dhidi ya Al Ahly nchini Misri, ambapo kadi yake ya njano ya kwanza aliipata katika pambano la marudiano dhidi ya APR Uwanja wa Taifa Dar es Salaam .
Kwa upande wa Kamusoko mwenye mabao mawili, alioneshwa kadi ya njano katika mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly pamoja na pambano la kwanza dhidi ya Cercle de Joachim.
Hata hivyo, kukosekana kwa wachezaji hao si pigo sana kwani kocha wa Yanga, Hans Pluijm ana hazina ya wachezaji ambao amekuwa akiwaanzisha katika mechi mbalimbali za ligi hiyo hivi karibuni, huku akiwaanzisha benchi Ngoma na Kamusoko.
Malimi Busungu ama Paul Nonga mmojawapo anaweza kuchukua nafasi ya Ngoma, huku ile ya Kamusoko akicheza ama Salum Telela, Mbuyu Twite, Said Juma Makapu au Haruna Niyonzima.
Yanga imeangukia katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1 Alexandria, Misri.

No comments:

Post a Comment