Wednesday, July 20, 2016

MOTO wateketeza mitambo kiwanda cha 21st Century

Kiwanda cha 21st century 
MOTO mkubwa umezuka Kiwanda cha nguo cha 21st  Century  kilichopo Kihonda Manispaa ya Morogoro na kuteketeza vitu mbalimbali ikiwemo baadhi ya mitambo ya kuzalisha nguo na  malighafi kiwandani hapo.


Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho Clement Munisi aliwaambia wanahabari mjini hapa kuwamoto huo ulizuka majira ya saa 12.00 asubuhi juzi katika  mashine moja ya kusuka vitambaa  ikitoa cheche  ambapo wafanyakazi waliokuwa zamu walipojaribu kuuzima kwa kutumia kifaa maalumu cha kuzima moto (Fire extinguisher ) ilishindikana.

Munisi alisema kuwa moto huo uliendelea kuenea katika vyumba vingine ndani ya kiwanda hicho na kusababisha baadhi ya nguo zilizokuwa zikiendelea kusukwa katika mitambo hiyo kuteketea vibaya na hasara yake haijafahamika mpaka sasa..

Kamanda wa kikosi cha zimamoto  Mkoa wa Morogoro Ramadhani  Pilipili  alisema kuwa licha ya kuwahi kufika mapema katika eneo la tukio na juhudi za kuuzima moto zikiendelea lakini bado miundombinu ya kiwanda hicho bado imekuwa  ni  kikwazo .

Kwa upande mwingine  Kamanda huyo alitoa wito kwa uongozi wa kiwanda kuhakikisha wanaweka miundombinu ya mabomba juu ya paa ili ikitokea tena tatizo kama hili iwe rahisi kushughulikiwa  ikiwemo uzimaji  moto.

Afisa Mazingira wa kiwanda hicho Anna  Gerevas alisema kuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho wako hatarini kukosa ajira kutokana na uharibifu uliosababishwa na moto huo  jambo linaloweza kupelekea kiwanda hicho kufungwa kwa muda na wafanyakazi kubaki majumbani.

hata hivyo baadhi ya wafanyakazi waliwabainishia wanahabari kwa sharti la kutotajwa majina yao wakisema kuwa mashine hizo zimekuwa zikitoa cheche kwa muda mrefu wakibainisha kuwa hiyo ni mara ya tatu kutaka kulipuka na kuzimwa mapema.   


No comments:

Post a Comment