Thursday, September 1, 2016

SERIKALI nchini Tanzania yashauriwa kutumia tafiti za wataalamu kukabiliana na changamoto za uchumi

SERIKALI imeshauriwa kutumia tafiti na hazina ya wataalamu vijana walio na wanaohitimu vyuo kuboresha na kukabiliana na changamoto za uboreshaji uchumi nchini kwa kasi inayokusudiwa katika maendeleo.


Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Rais wa wanafunzi kutoka Kampasi kuu ya Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro Yona Abiya  wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipokuwa ikifungua jumuiya ya wanafunzi wa kodi vyuoni, chuoni hapo.

Abiya alisema kuwa wanafunzi wana nafasi kubwa ya kuweza kutoa elimu kwa jamii ikiwemo wanafunzi wenzao na kufanya elimu hiyo kwa mlipakodi kulifikia mapema Taifa.

Aidha Abiya alisema, wanafunzi vyuoni wanayo nafasi kubwa kuweza kubadilisha Taifa lenye kutamani maendeleo bila kusahau kuwa maendeleo yoyote yanakuja kwa gharama ikiwemo ya wao wenyewe kulipa kodi Serikalini.

Hata hivyo aliwasishi wanavyuo kutumia nafasi hiyo kujiunga na umoja huo na kuonesha ushiriki kikamilifu wakiwa na lengo moja la kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuhamasisha jamii kudai risiti baada ya kununua bidhaa ili kuimarisha makusanyo ya kodi sambamba na kuwafanya wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kuweka kumbukumbu.

Naye Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi (TRA) Richard Kayombo aliwataka wanafunzi kuwa makini na masuala ya manunuzi hasa katika suala la kutoa na kudai risiti ili kuwezesha Serikali kuendeleza mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo suala la uboreshaji wa mikopo ya wanafunzi.

Aidha Kayombo alisema kuwa mikopo inayotolewa kwa wanafunzi hutolewa kwenye kodi za wananchi na kwamba ikiwa vijana watajenga nia na moyo wa kulipa kodi watawezesha Serikali kufanya mambo mengi ya maendeleo inayokusudia 

No comments:

Post a Comment