Thursday, April 17, 2014

RAISI JAKAYA Kikwete akemea tabia ya baadhi ya watu kuwakejeli waanzilishi wa Taifa la Tanzania



RAISI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu kwa baadhi ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli Waanzilishi wa Taifa la Tanzania, Hayati Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa viongozi hao wawili wameifanyia Tanzania mambo mengi, mambo makubwa na mambo ya kihistoria kiasi cha kwamba Watanzania wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa namna ya kudumu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu,jijini  Dar es salaam,Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari usiku wa jana, Jumatano, Aprili 16 katika mahojiano maalum ya kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano.

Rais Kikwete amesisitiza kuwa ni ukosefu wa adabu kwa yoyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu matusi, kejeli, dhihaki ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na Wabunifu Wakuu wa Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment