Wednesday, May 7, 2014

BIASHARA ndogondogo milioni tatu nchini hazijasajiliwa




SERIKALI imeshauriwa kuboresha mifumo ya usajili wa biashara, ili kurahisisha wajasiriamali wengi kusajili biashara zao na kuliwezesha Taifa kupanua wigo wa ukusanyaji mapato.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ivestment Climate Facility for Africa (ICF) Bw William Asiko, akizungumza na wajasiriamali wadogowadogo zaidi ya mia saba waliokutana jijini Dar es salaam,jana amezishauri mamlaka zinazohusika, kumsaidia mjasiriamali kuondokana na vikwazo vya kibiashara, sambamba na kuwataka wajasiriamali waliopatiwa mafunzo kuwa na utamaduni wa kusajili miradi yao ya kibiashara ili waweze kutambulika kwenye taasisi za kifedha na kuwawezesha kupata mikopo ya kuendeleza miradi yao..

Kwa mujibu wa taasisi hiyo yenye lengo la kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa wajasiriamali barani Afrika,   inasadikiwa kuna biashara ndogondogo milioni tatu nchini ambazo hazijasajiliwa kisheria.

Kwa mujibu wa Taarifa rasmi za serikali wakati wa maadhimisho ya siku ya viwanda Afrika Novemba 20 mwaka jana, sekta ya wajasiriamali wadogo ina viwanda vidogo vidogo zaidi ya milioni  tatu ambavyo vinaajiri zaidi ya Watanzania milioni 5.2 huku mchango wake katika Pato la Taifa ukiwa ni asilimia 27 na kwenye ajira ni asilimia 23.4 ya nguvu kazi yote nchini.

No comments:

Post a Comment