Tuesday, May 6, 2014

KAMPUNI ya Alliance One yatoa msaada wa vyakula wenye thamani ya shilingi milioni tano kwa waathirika wa mafuriko


UONGOZI wa kampuni ya kusindika Tumbaku ya Alliance One Tanzania Limited ya mjini Morogoro umetoa msaada wa vyakula wenye thamani ya shilingi milioni tano kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wa Wilaya ya Morogoro.

Akizungumza katika makabidhiano ya msaada huo uliotolewa jana mbele ya mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bwana Saidi Amanzi,meneja mahusiano wa kampuni hiyo,Bwana Hamisi Liana,amesema kuwa kampuni hiyo imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuwa zaidi ya kaya 1396 zenye jumla ya watu 6986 ndani ya wilaya hiyo zimeathirika na mafuriko hayo.

Aidha Bwana Liana amesema kuwa mafuriko ni janga ambalo hutokea mahali  popote na wakati wowote hususani wakati wa mvua nyingi kama ilivyotokea kwa wakazi hao wa wilaya ya Morogoro na kusababisha hekta zipatazo 2778 za mazao mbalimbali kuharibika.

Sambamba na hilo amesema kuwa kampuni ya Alliance One itaendelea kushirikiana na uongozi wa serikali wakati wote itakapohitajika kufanya hivyo,huku akiwaomba watanzania na makampuni mbalimbali kushiriki katika kuwasaidia watu hao waliopatwa na janga hilo la mafuriko.

Msaada wa vyakula uliotolewa ni mifuko 100 ya unga wa sembe yenye kilo 25 kila mmoja,kilo 1000 za maharage pamoja na lita 200 za mafuta ya kupikia.

No comments:

Post a Comment