Sunday, May 4, 2014

RAISI Kikwete ameitaka sekta binafsi kujihusisha zaidi katika mapambano dhidi ya ukimwi



RAISI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka sekta binafsi kujihusisha zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa sababu ugonjwa huo unaathiri uchumi na biashara na kuongeza mzigo wa gharama za uzalishaji wa makampuni hayo.
   
Kwa mujibu  wa taarifa iliyotolewa jana  na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Kikwete amesema  kuwa pamoja na kwamba Tanzania imekuwa inapata michango mikubwa ya  kupambana na UKIMWI kutoka kwa washirika wake wa maendeleo, bado jukumu la msingi la kupambana na ugonjwa huo nchini ni la Watanzania wenyewe. 
     Pia, Rais Kikwete amewakumbusha Watanzania kuwa UKIMWI hauna tiba ya kisayansi ama tiba mbadala ya waganga wa jadi ama wapiga ramli kama baadhi ya Watanzania wanavyopenda kujiaminisha. 
   
Rais Kikwete alikuwa anazungumza hayo usiku wa kuamkia, Jumamosi,wakati alipokuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya uzinduzi wa uchangishaji fedha za kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya mapambano ya UKIMWI kwa mwaka huu wa 2014 kwenye Hoteli ya  Regency jijini Dar es Salaam.
Katika shughuli ya usiku huo, Rais Kikwete alitoa hundi ya shilingi milioni 700 kwa taasisi mbali mbali kutokana na fedha zilizokusanywa mwaka jana chini ya mpango huo wa Kili Challenge.


No comments:

Post a Comment