CHAMA cha madaktari rafiki wa Ifakara,mkoani Morogoro kwa kushirikiana na shirika la
MIVA toka nchini Austaria wameikabidhi hospitali ya rufaa ya Mt.Francis gari la
kubebea wagonjwa lenye thamani ya shilingi milioni 61.8.
Makabidhiano ya gari hilo aina ya
Landcriser yamefanyika jana katika hospitali hiyo mbele ya uongozi wa hospitali
hiyo chini ya askofu wa jimbo la Ifakara Mhashamu Salitaris Libena
na Rais wa Chama cha madaktari rafiki wa Ifakara Dr Willi Schennach na
wafanyakazi wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk
Angelo Nyamtema alisema kuwa chama hicho cha madaktari rafiki wa Ifakara
kimeanza kuisaidia hospitali hiyo kwa miaka 20 sasa kwa kuwapatia vifaa
mbalimbali ikiwemo jenereta,mashine za kufulia,vifaa tiba,fedha na kusomesha
madaktari bingwa katika hospitali hiyo na pia kuleta madaktari bingwa kutoka
nchini mwao kuja kubadilishana utaalamu na madaktari wa hospitali hiyo.
Dk Nyamtema alisema msaada wagari
hilo umekuja wakati muafaka kwani gari la mwanzo halikuwa na vifaa muhimu ila
la sasa limekamilika na litasaidia kwa wagonjwa mahututi kuwapelekea katika
hospitali nyingine kubwa kama ikitokea dharura.
Alisema kuwa hospitali yoyote
inayotoa huduma bora lazima iwe na gari la uhakika la wagonjwa hivyo kuwaahidi
wafadhili hao kuwa gari hilo jipya walilopewa watalitumia kwa malengo
yaliyokusudiwa na sio katika shughuli nyingine.
Kwa upande wake askofu wa jimbo la
Ifakara Mhashamu Libena alisema mchango wa gari la wagonjwa ni habari
njema si tu kwa hospitali bali pia kwa jamii katika huduma pana zaidi ambapo
huduma hii itaokoa maisha kwa wagonjwa wengi hivyo kuwapongeza wafadhili hao
wawili kwa ukarimu wao na kuwaomba kuendelea kuwasaidia kama walivyoanza
tokea miaka 20 iliyopita.
No comments:
Post a Comment