Wednesday, June 25, 2014

IRAN yalaani shambulio la kigaidi nchini Lebanon


Bi Marzieh Afkham ,msemaji wa wizara ya mambo ya nje nchini Iran

JAMHURI ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulio la kigaidi lililotokea Jumatatu nchini Lebanon, na kusema kuwa ni sehemu ya njama za Israel zenye lengo la kuchochea makundi yenye misimamo ya kupindukia mipaka na migogoro ya kimadhehebu katika eneo la Mashariki ya Kati.


Marzieh Afkham msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kwamba, bila shaka mataifa ya eneo hilo hasa Lebanon yataimarisha umoja, mshikamano wa kiataifa na kuzima njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuwakingia kifua magaidi na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada.

Jumatatu usiku mlipuko wa kigaidi ulitokea kusini mwa Beirut mji mkuu wa Lebanon na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na kujeruhiwa.
Umoja wa Mataifa pia umelaani shambulio hilo na kulitaka taifa la Lebanon kuimarisha umoja katika kupambana na ugaidi.

No comments:

Post a Comment