Mtambo wa Tanesco Kihansi, Kilombero, Morogoro |
HATIMAE mgogoro
wa ardhi uliodumu kwa karibu miaka 20 kati ya wananchi wa Mlimba na shirika la
umeme nchini(Tanesco) tawi la Kihansi umetatuliwa na halmashauri ya wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Katika mkutano wa mapatano pande hizo mbili,kaimu mkurugenzi wa
halmashauri hiyo Jackson Mpankuli alisema wameamua kuingilia kati kupata ukweli
na kumaliza tatizo hilo.
Alisema hatua baada ya mazungumzo hayo ni wananchi kupitia kamati
waliyoiunda kusimamia mgogoro huo kwa kuanza upya maombi ya ardhi wakieleza
mahitaji yao toka katika eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 28 kwakua ni eneo
halali la Tanesco.
Kaimu mkurugenzi huyo alisema kuwa wao kama halmashauri
watashirikiana na wananchi katika maombi hayo ili kuhakikisha eneo linapatikana
na shughuli za maendeleo zinafanyika eneo moja huku eneo lingine likibaki kwa
Tanesco Kihansi.
Awali mwenyekiti mstaafu kijijini hapo Benard Namhongoma alitoa
histora fupi ya shirika hilo kupata eneo hilo akisema kijijini hapo mwaka 1994
akisema walifuata hatua zote za kisheria wakati huo na waliokutwa eneo hilo
walilipwa fidia.
Namhongoma alisema wao waliridhia na kuomba wananchi waliokuwepo
eneo hilo ambao walikuwa wakiliendeleza kwa shughuli za makazi na kilimo kutoka
na kuwapisha Tanesco na shirika lilianza ujenzi wa hospitali ambayo ipo hadi
leo.
Aliongeza kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa alipoagiza hospitali
hiyo irudishwe kwa wananchi shirika lilikubali na lilibaki eneo hilo kwa ajili
ya nyumba za watumishi na sio kweli kwamba eneo hilo waliwapa Tanesco kwa ajili
ya makazi binafsi ya watumishi.
Kwa upande wake meneja wa Tanesco Kihansi Pakaya Mtemakaye alisema
shirika hilo wanamiliki eneo hilo kihalali na waliwalipa watu wote waliowakuta
eneo hilo kwa kufuata sheria ya mwaka ule na ofisi yake haina lalamiko la madai
na anashangaa kusikia kuwa kuna watu wamepewa eneo hilo.
Nae afisa ardhi na maliasili wa wilaya Sakurani Mushi alisema
wakati serikali inaomba eneo hilo sheria iliyotumika ni ya mwaka 1923 na fidia
iliyotumika ni ya mwaka 1967 na malipo yalifanyika bila malalamiko kuhusu fidia
na Tanesco wana hati miliki halali ya eneo hilo.
Mushi alisema wakati Tanesco wanaomba eneo hilo waliomba kwa ajili
ya nyumba za wafanyakazi,viwanja vya michezo na hospitali na kwa sasa
wamejipanga upya kwa kutaka kujenga makazi yao na hawana kosa kwa kujipangia matumizi
katika eneo lao.
No comments:
Post a Comment