Wednesday, March 30, 2016

WALIMU Morogoro wahofia usalama wa afya zao .

WALIMU walio shule za msingi kata mpya ya Kibuko tarafa ya Mkuyuni Wilayani Morogoro wanakusudia kuachana na kazi hiyo kisha kujishugulisha na kazi nyingine ikiwemo biashara kutokana na hofu ya usalama wao kiafya.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na timu ya waandishi wa habari iliyotembelea vijiji vya kata hiyo kwa ushirikiano na mtandao wa jinsia nchini TGNP walimu hao walisema kinachowakatisha tamaa ni kutelekezwa vijijini humo bila huduma muhimu licha ya huduma ya maisha wanaopambana nayo kila kukicha.

Mbali na uduni wa nyumba hizo, waandishi walishuhudia ukosefu wa vyoo,maji na kuwalazimu walimu kutumia muda mwingi kusaka huduma hizo huku baadhi ya familia za walimu hao wakilazimika kuchangia choo kimoja na familia nyingine kutumia vyoo vya shule.

Walisema kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiishi mazingira magumu yakiwemo ya kudhalilika jambo linalowaathiri kisikolojia na kufifisha juhudi zao za kufuta ujinga kwa watoto ambao ni  Taifa la kesho.

Awali kwa nyakati tufauti wenyeviti wa kamati za shule ikiwemo ya Luholole Shiwa Chalo na shule ya msingi Kibuko Kasimu Ramadhani  walieleza kusikitishwa na serikali kushindwa kuunga mkono juhudi za wanachi katika kuboresha maendeleo hususani katika miundombinu ya huduma ya jamii kama shule na afya.


Kata ya Kibuko ni mpya iliyopatikana kutoka kaya na tarafa ya Mkuyuni wilayani Morogoro na inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ofisi na nyumba za walimu,uwekezaji holela katika madini,misitu,maji na miundombinu ya barabara kwa miaka mingi.

No comments:

Post a Comment